Lulu sasa abadilishiwa mashtaka
MSANII
Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, ameepuka adhabu ya kunyongwa hadi
kufa kwa tuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba baada ya
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kumbadilishia mashtaka, ambapo sasa
anatuhumiwa kuua bila kukusudia. Kutokana
na mabadiliko hayo, Lulu ameepuka adhabu hiyo kwani hata kama
atapatikana na hatia, adhabu yake ni kifungo cha maisha au kuachiwa
huru.
Hii
inatokana na kifungu cha 196 cha kanuni za adhabu ya kosa la kuua bila
kukusudia, ambapo anayepatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha
maisha, miaka kadhaa au kuachiwa huru.
Hata hivyo,
baadhi ya wanasheria waliliambia gazeti hili kwamba uzoefu wa adhabu
nyingi za kuua pasipo kukusudia zilizowahi kutolewa nchini, ni kati ya
miaka 15 na wengine waliachiwa huru.
Lulu alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aprili 11, mwaka huu akikabiliwa na tuhuma za kumuua Kanumba Aprili 7, 2012.
Alikuwa
akidaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), shtaka ambalo mshtakiwa anayepatikana
na hatia adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.
Hata hivyo,
jana upande wa mashtaka ulieleza mahakamani kuwa kwa sasa imebadilisha
mashtaka kutoka kuua kwa kukusudia na kuwa kuua bila kukusudia, kinyume
cha kifungu cha 195 cha CP.
Mshtakiwa
huyo alitarajiwa kusomewa mashtaka hayo mapya jana pamoja na maelezo
yote ya kesi, ambapo angesomewa ushahidi wa mashahidi wote pamoja na
vielelezo muhimu katika kesi hiyo.
Hata hivyo,
hatua hiyo ilikwama kutokana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini
Kweka anayeiendesha kesi hiyo kutokuwapo mahakamani na badala yake
aliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Ofmedy Mtenga.
“Upelelezi
wa shauri lako umeshakamilika na tungeweza kukusomea comital (maelezo ya
kesi) leo, lakini kwa kuwa waendesha mashtaka hawapo basi
tunaliahirisha mpaka tarehe nyingine.”, alisema Hakimu Mkazi Agustina
Mmbando, anayesikiliza kesi hiyo katika hatua hiyo ya awali.
Taarifa hizo
za kukamilika kwa ushahidi wa kesi hiyo zilipokewa kwa furaha na
shangwe na msanii huyo, kiasi kwamba alishindwa kujizuia kuonyesha
furaha yake.
Wakili
wake Peter Kibatala aliiomba mahakama itoe ahirisho fupi hadi Ijumaa
kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa mashtaka haya mapya pamoja na maelezo ya
awali.
Hakimu Mmbando alikubaliana na ombi hilo la Wakili Kibatala na akaahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa.
Baada ya Mahakama ya Kisutu kukamilisha taratibu hizo kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu ambako ndiko itakaposikilizwa.
Lulu
alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili 11,
2012 na kusomewa shtaka moja la mauaji ya msanii mwenzake, Kanumba.
No comments:
Post a Comment